Wednesday, August 3, 2011

NIMLILIE NANI...


Matochi ndilo jina alilojulikana zaidi karibu kila pande za dunia. Wengi walimfahamu kwa jina hilo la kimajazi ukiachilia mbali na jina kamili alilopewa na wazazi wake. Chakushangaza wazazi hawakulitambua ingawaje wengi waliomjia hata nyumbani kwao wali mwita vile. Pengine walipuuzia kwa kudhani ni lugha ya mtaani tu au labda ilikuwa isimu na namna ya ngeli ngumu zitumikazo mitaani hosusani na vijana jamii yao. Jina kamili alilopewa na wazazi baada ya kubatizwa lilikuwa Juhudi Majaaliwa.
Alizaliwa tarehe 24 mnamo mwezi wa tisa 9 mwaka 1983 kando ya shamba kubwa la kahawa lililoitwa Mashon mkoani Arusha. Mashon lilikuwa jina la mkoloni wa kwanza aliyetoka ujerumani ambaye alimiliki shamba lile la kuzalisha kahawa. Lakini hatahivyo ukuwaji wa mji wa arusha toka ngazi ya vijiji mitaa na vitongoji viliambatana na ongezeko la watu miaka ya 60 ambapo Tanganyika kwa wakati huo ilipata uhuru toka mikononi mwa waingereza walioichukuwa sehemu ya afrika mashariki baada ya maamuzi ya mkutano uliofanyika huko ujerumani kuligawa bara la afrika maarufu kwa jina la Berlin conference 1884/1885. Pia mikutano mingine ya kuzigawa sehemu za bara hili iliyofanyika enzi za wakoloni zifaamikazo kama ‘scramble and partition of Africa’. Jina la Moshono ndipo lilipochimbuka hasa kutokana na kumbukumbu ya vizazi na vizazi ambavyo vilishuhudia au kufanyishwa kazi kwenye mashamba yale.
Majaaliwa na Dorothea walikuwa wenyeji wa Kilimanjaro wilaya ya Moshi vijijini lakini kwa bahati mbaya au nzuri waliloweya mkoani arusha kwa sababu za kijamii kisiasa ama kiuchumi. Wakati haya yakiendelea ilikuwa mwaka 1968 ndipo wawili hao walipokutana wakiwa shule middle school kwa wakati huo. Hatahivyo mahusiano mema huzaa mema kama ilivyo ada wakazaliwa watoto watano na kuifanya familia iliyo sheheni furaha na Baraka. Wa kwanza alikuwa msichana aliyeitwa Sia akifuatiwa na mwanaume aliyeitwa Yusufu. Wengine ni Haika, Juhudi na Benguo. Ilikuwa Baraka na kudura za maulana kwa kuwatoa watoto hao makusudi kwa wapendanao hao wawili yaani baba na mama Majaaliwa. Penye wengi hapaharibiki neno kama wasemavyo wahenga katika jopo la watoto watano lazima angelitoka moja kati yao mwenye mwenendo mzuri kitabia, kiakili na baadae kuwa na uwezo na mafanikio katika maisha.
Akiwa mtoto wa pili kutoka mwisho Juhudi alipendwa sana na baba na mama yake kwani alionekana kuwa nyota njema tena yenye nguvu. Alikuwa mwerevu mpole sana mwenye huruma na juhudi nyingi muda wote alionekana kimya akitafakari.mbali na wasifu huu juhudi alikuwa mtoto mwenye hasira za karibu, akupenda kabisa kubughuziwa. Juhudi alikuwa mithili ya taswira ya babake mzee Majaaliwa. Walifanana kwa kila kitu. Japo ni jina la kimajazi lakini liliwiana sawa sawiana tabia yake ya kupenda kila palipokuwa na kazi. Tabia yake ya huruma ilionekana pale alipokuwa akicheza na mdogo wake Benguo wakati mama yake alipokwenda kazini. Mama majaaliwa alikuwa mwalimu katika moja ya shule za msingi iliyokuwa jirani. Katika kipindi chote cha utoto wake Juhudi hakupenda michezo kama ilivyo kwa watoto wengine, alikaa karibu na mdogo wake Benguo na kuigiza kila kilichofanywa na wakubwa. Mzee Majaaliwa alipenda kuongozana nae kila pembe jambo lililowashtua nduguze wengine kwani hawakuwahi kupata kuwa karibu zaidi na baba yao kama ilivyokuwa kwa Juhudi.
Kwa upande mwingine Mzee Majaaliwa alikuwa na mke pamoja na watoto wengine saba. Mama Lii lilikuwa jina la mkewe wa kwanza aliyekuwa mama wa nyumbani. Juhudi hakuwahi kufikiri kwanini wazazi waliishi kwa chuki, kelele, fitina na pia ugomvi kila kukicha. Ukiachia mbali udogo wake asingeliweza kufikiri hivyo kwani alikuwa kipenzi cha wote hivyo penye ugomvi hapakumhusu kamwe. Mze Majaliwa alikuwa mwingi wa hasira na mwepesi kuunyanyua mkono wake kumwadhibu aliyembughuzi. Wakati mwingine alihifadhi jambo na kutegea magharibi ifike ili aweze kuitoa hadhabu yake barabara. Alipenda kujiunga na wazee wenzake kila jioni wakipata viburudisho kwenye vilabu vya pombe. Alikuwa mlevi aliyekunywa bandika bandua ilimradi kipato chake kilimruhusu. Sifa umaarufu vilimwenea ukichukulia heshima aliyopewa kwa kuwa mfanyakazi wa serikali civil servant tena katika sekta nyeti yaani wizara ya ujenzi.
Majaaliwa alikuwa na shehena ya mlimbiko wa mali tele ijapokuwa wakati wa Mwalimu Nyerere ilikuwa haramu. Kurupushani na migogoro iliyokuwa katika familia hii haikuhusishwa na njaa au ukosefu wa chakula wala mavazi. Bali vilikuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotokana na aidha udini, umbile au chuki zilizosababishwa na mchanganyiko wa pande mbili zenye uadui. Hii ni kwasababu kimaadili wakristo hawaruhusiwi kuoa mke zaidi ya moja. Kwa hakika wanawake hasa ndio waliosambaratishana na kutupiana lawama kila siku ya mungu. Juhudi alihisi labda mamaye ndiyo alikuwa mkosefu kwani pindi alipokuwa kazini palikuwa shwari. Kiukweli mama Juhudi alikuwa msemaji sana hakuchoka kuongea yaliyomkera. Wakati mwingine alidiriki kutishia kuondoka katika nyumba yao ambapo walikaa na mke mwenza.
Wakati haya yakiendelea Juhudi alikuwa na kadirri ya miaka minne tu, hakika tayari alishaanza kujua ya walimwengu. Usemi wa dunia tambara bovu ulimwingia kinda huyu pale mama Dorothea alipoamua kuuama mji na kwenda kusikojulikana. Aliporomosha madai bila breki; kwanza amechoshwa na ukatili wa mama Lii na visa vyake pia ubishi na umwamba wa mzee Majaaliwa. Dorothea aliacha watoto wake wote watano kwa mumewe na kuchukua kila kilichokuwa chake. Kilichowasikitisha wengi ni Benguo aliyekuwa na umri wa mwaka moja na miezi tisa tu. Ulikuwa mwaka wa uchungu kwa watoto wale lakini mwaka wa furaha kwa upande wa pili yaani kwa mama Lii. Alimradi mbaya wake aliondoka, alikubali kulea watoto watano bila kinyongo. Alijisifu kila kona kwamba yeye shujaa tena mwenye msimamo mkali zaidi ya mwanajeshi vitani aliyekula lilambo na kiapo kumshinda adui kwa kumwangamiza vikali mno.
Mzee majaaliwa alikubali hali hile na kuonya asinge mrejesha tena mkewe katika nyumba ile kwa kitendo cha kinyama alichokifanya. Alijisikia hasira kila alipowatazama watoto wake watano wakiwa na kuona haibu kwa tendo la wanawe wale kulelewa na mama Lii. Hakuna masika yasiyo na mwisho uchungu ulisahaulika kwa muda na kupisha majukumu mengine kuendelea.
Majaaliwa aliamua kumuanzisha Matochi shule ya awali mwaka 1989 kwani nduguze wote walikuwa wakisoma katika shule ya msingi iliyokuwa jirani. Miaka miwili tangu kutoweka kwa Dorothea ambaye hakujulikana aliko zaidi ya tetesi ya kwamba aliamua kujishughulisha na biashara ndogo ndogo mjini Arusha.Matochi alianzishwa darasa la kwanza katika shule ya msingi Moshono. Lengo la mzee majaaliwa lilikuwa kuhakikisha kuwa watoto wake wote wanapata elimu ambayo ni bora kwa manufaa yao ya baadae.
Waalimu na wanafunzi walimpenda sana Matochi kwa jitihada zake katika masomo na pia ushirikiano aliokuwa nao kwao. Alichaguliwa kuwa kiranja wa darasa. Mzee majaaliwa alizidi kuwa na furaha juu ya mafanuikio ya mwanae pale matochi alipofaulu kwa kiwango cha juu zaidi ya wote kwenye mitihani ya mwisho wa muhula.
Lilikuwa pendekezo kutoka kwa bodi na kamati ya shule kumteua mzee majaaliwa kuwa mwenyekiti wa shule ile. Alipewa nafasi ile kutokana na kuonekana mfano wa kuigwa kwani alikuwa karibu sana na waalimu kufuatilia maendeleo ya wanawe. Kitumbua kiliingia mchanga palejuhudi alipo kumbuka umuhimu wa kuwepo kwa mama yake. Alifanya kila njia kusahau lakini ilikuwa sawa na kulijaza nafaka gunia lenye matundu.
Mama yake Dorothea alianza kujitokeza nyumbani kuwasabahi wanawe lakini haikuwa kazi rahisi kwake kufanya hivyo kwani alipata vikwazo toka kwa mama Lii aliyepewa dhamana ya kuwalea Matochi na nduguze. Matochi alipotoka shule alibadili nguo kasha kula chakula cha mchana na aliwajibika na kuangalia mifugo. Aliwachunga mbuzi kando kando ya mashamba ya mzee majaaliwa. Ilipofika jioni aliifungia mifugo na kasha kuoga na kutayarisha vitabu pamoja na mavazi yake ya shule. Baada ya kula chakula cha jioni Matochi alijikumbusha kwa kusoma aliyofundishwa. Mbali na baba yake kuwa na luninga Matochi hakuwa na desturi ya kutizama luninga katika siku za wiki isipokuwa mwishoni mwa wiki tu.
Kaka yake Yusufu hakupenda shule alikorofishana na waalimu na mzee Majaaliwa kila kukicha. Hakujua kuunganisha mbili na mbili upate nne. Wakati mwingine kabla ya masomo kuisha alitoroka shuleni kwenda kuzurura mitaani. Ilipofika saa ya kurudi nyumbani alijiunga na wenzake huku akijifanya ametoka masomoni. Taarifa ilipotumwa kwa mzee Majaaliwa kutoka kwa waalimu Yusufu alitoroka nyumbani na kwenda kwa rafiki zake ambako alisubiri kiza kingie. Hakupenda kuoga wala kufanya usafi kwa ujumla. Hakupenda kufanya kazi za nyumbani wala zile alizopewa na waalimu wake shuleni. Hakika alikuwa mtukutu asiye na adabu wala utii kwa walimu na wazazi. Yusufu alipenda zaidi kazi za kuendesha magari. Kwa wakati wote alijishughulisha na madereva wa trekta na magari ya babake. Sia yeye alifanya mitihani ya kuitimu elimu ya msingi hivyo alisubiri matokeo. Haika alikuwa darasa la tatu. Kwa bahati mbaya matokeo ya sia hayakuwa mazuri. Mzee Majaaliwa aliazimia kumtafutia shule ili arudie mitihani. Alipopata shule wilayani Serengeti aliwapeleka sia na yusufu aliye amishwa kutoka shule ya msingi Moshono.
Benguo yeye alibaki nyumbani na mama Lii. Aliweza kuifungulia mifugo kwenda malishoni na kuirudisha. Pia aliweza kufanya kazi nyingine kama vile kwenda dukani kununua vitu vidogo vidogo. Benguo alikuwa mpole sana hakupenda kusema maneno mengi. Wakati mwingine akihojiwa aliitikia kwa kichwa. Alinunu liwa ubao mweusi wakuandikia kwa chaki. Aliutumia zaidi kuchora picha kwani alipenda sana fani ya uchoraji.
Alipofikisha umri wa miaka kumi Matochi aliipenda sana fani ya muziki. Aliweza kuwa tambua baadhi ya wanamuziki wa ng’mbo ambao walijipatia umaarufu sana kwa wakati huo kupitia luninga. Alipenda kuigiza na kuimba nyimbo za mwimbaji aliyejiingiza katika muziki akiwa kinda kutoka nchini Marekani aliyeitwa Michael Jackson. Alikuwa msanii chipukizi aliyetetemesha anga za muziki pande nyingi duniani. Kilichomvutia Matochi ni unadhifu wa mavazi na uwezo mkubwa wa kucheza aliokuwa nao Michael Jackson. Alikuwa nyota katika bendi iliyosheheni wanafamilia ya The Jacksons. Mzee majaaliwa alikitambua kipaji hicho kutoka kwa mwanae lakini hakupenda mwanae kujihusisha na muziki. Kwa wakati huo muziki ilikuwa fani ya wahuni wasio na elimu wala utii.
Matochi alianza mafunzo ya kipaimara katika kanisa lililokuwa jirani na makazi yao la Moshono akiwa darasa la saba. Miezi michache baadae alihitimu elimu ya msingi kwa kufanya mitihani ya kumaliza darasa la saba. Mwishoni mwa mwaka 1998 alihitimu pia mafunzo ya kipaimara katika kanisa la Moshono. Kutokana na juhudi zake katika masomo hayo aliweza kuonekana mwanafunzi bora. Mwalimu wake aliwatunuku zawadi yeye na wenzake wane ambao pia walifanya vema kwenye mitihani na majaribio ya somo la dini siku ya kubarikiwa.
Mwanzoni mwa mwaka 1999 masikio na macho yalielekezwa kwenye vyombo vya habari kujua mustakabali wa matokeo yaliyotangazwa na baraza la mitihani Tanzania. Kwa bahati mbaya yalitangazwa majina nane tu. Kati yao hapakuwa na jina la Matochi. Mzee majaaliwa aliazimia kwenda kuchunguza kujua kwanini jina la mwanae halikuwapo. Asubuhi ya siku iliyofuata mzee Majaaliwa alimwendea katibu afisa elimu wa mkoa. Pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watu waliosubiri huduma mzee Majaaliwa alifanikiwa kuonana na katibu Yule. Baada ya kupewa kitabu chenye majina ya wahitimu waliopaswa kuchaguliwa mzee Majaaliwa alishangaa kuona jina la mwanawe. Kulikuwa na majina mengine ya wanafunzi wanne toka Moshono. Wazazi wote waliofika kwa shida ya kujua ksababu ya kutochaguliwa wanao kwa wakati ule waliitwa na Afisa elimu wa mkoa. Waliambiwa wawe na subira kwani kuna tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule ya kutwa Arusha. Hivyo ingelichukua takribani mwezi mmoja kumalizika zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa. Mzee Majaaliwa alimpeleka Matochi katika shule ya mafunzo ya lugha za kigeni ya Molac. Huko alijifunza lugha ya kiingereza.
Haikuwa shinikizo kubwa kwao kwani Matochi alifanya vizuri na kupita mitihani ile. Ilikuwa furaha isiyo na kifani kwa mzee majaaliwa na familia yake. Mzee majaliwa alihaidi kumpeleka shule yeyote ama bweni ama ya kutwa kama moja ya zawadi zitakazo shinikiza mchakato wa mafanikio yake.
Mama Lii alionesha furaha usoni tu lakini moyoni alichukizwa sana na kitendo kile. Kwa ukweli alikubali kuwalea tu watoto wale kwa kuwapa malezi duni ilimradi wasifanane na wanawe. Hakula chakula cha jioni siku ile badala yake aliigiza kuumwa. Alidiriki kuwanyamazisha wote waliosheherekea kwa kuongelea kufaulu kwa Matochi. Hata hivyo siku ilipita watu wakalala na kuamkia siku ingine.
Barua ya kujiunga na shule ya kutwa ya Arusha ilitumwa kwa mzee Majaaliwa ikiambatana namahitaji ya vifaa muhimu vya kununua. Mzee Majaaliwa alitimiza kama barua ilivyoagiza kwa kununua mahitaji yaliyobainishwa.
Shule ya kutwa ya Arusha iko kilometa saba toka Kijiji cha Moshono. Kutokana na tatizo la usafiri wa kutoka kijijini pale hadi mjini kuwa sugu mzee majaaliwa alibuni mbinu ya kulitatua tatizo lile. Alimtaka Matochi aamie kwa mjombake aliyeishi mjini kando na shule ya kutwa ya Arusha. Haikua kazi rahisi kwa Matochi kukubali kuishi na mjombake. Hakuwahi kusafiri wala kuishi kwa ndugu yeyote toka udogo wake. Alimwomba baba yake amnunulie baisikeli ili aendelee kukaa nyumbani pale. Mzee Majaaliwa alikubali kishingo upande kwani alihofu mwanawe angeweza gongwa na magari kule mjini.
Matochi alianza kuishi maisha mapya baada ya kukutana na wanafunzi wenzake katika shule ya sekondari. Wengi huamini sekondari ni utu uzima. Wanafunzi wengi wa sekondari hujiita wapevu kimwili hata kiakili. Lakini kwa Matochi yalikuwa maisha mapya hasa. Alikuwa mshamba asiyejua ya mjini. Alishangazwa na kustaajabu ya mjini. Aliyapenda sana maisha ya shule. Alijua bidii ndio ingemfanya aweze kuendelea kusoma hadi chuo kikuu. Hivyo alikuwa makini sana na masomo.
Upole na umakini viliwafanya wanafunzi wengi kumhadaa kwa maswali. Walipogundua ulikuwa upole asilia walikaa kimya. Walimu walitambua hili lakini hapakuwa na tatizo kwani pale alipotakwa kujibu maswali alijibu bila wasiwasi. Haikuwa vigumu ijapo kuwa masomo yalikuwa kwa lugha ngeni ya kiingereza.
Matochi alikuwa na tabia ya woga kupita kiasi. Hakuweza kusimama mbele ya wenzake au katikati ya jopo la watu wengi. Haibu na soni vilimjaa. Ni udhaifu ambao bila shaka aliurithi aidha kwa baba au kwa mama. Hakuweza kujichanganya na jinsia tofauti na yake. Ikiwa wangewekwa kimakundi bila kujali jinsia alidiriki kutoongea chochote. Wanafunzi wenzake walimcheka na kutania kila walipofanya makongamano kwenye somo la kiingereza kwa kumtaka aende mbele kutoa hoja. Alipolazimishwa alijikokota taratibu huku wasiwasi ukimjaa. Alitokwa na kijasho chembamba na kupata kigugumizi cha ghafla. Viungo vilikosa nguvu na kutetema mithili ya mzee aliyefikisha miaka mia. Huu ndio udhaifu aliokuwa nao.
Hii ilikuwa mwanzo wa safari ya kuuaga utoto na kuukaribisha utuuzima. Wahenga wanasema utuuzima dawa kwani mtu hubadilika kitabia kwa kuziacha tabia za kitoto zisizo na maana na kuanza kupanga ya ukubwani. Wakati huu kila aliye mwona alitanabahi na kutoa tasmini kwa jinsi akili na mawazo yake yalivyomtuma. “Umekuwa mrefu, umekuwa mkubwa, umekuwa mtanashati, umekuwa na sauti nene”. Yalikuwa maneno ya wale waliomwona kipindi cha nyuma sana wakijaribu kulinganisha na wakati wa sasa.
Kwa kawaida sekondari ni ngazi ambayo mwanafunzi huwa na marafiki wengi wa jinsia zote. Alikadhalika kwake alikuwa na marafiki wa jinsia tofauti. Wapo aliokaa nao darasa moja wakisoma pamoja, wapo waliokuwa hawasomi nae bali waliishi mtaa moja pia wale wa shule jirani ambao alikutana nao aidha akiwa safarini kuelekea shuleni. Ujana una mambo mengi wapo waliosema ujana ni maji ya moto wengine wakisema ujana ni kama saruji mbichi ambayo hunasa chochote kitakachoidondokea.
Sio siri Matochi alikuwa na msimamo mzuri kimasomo hali iliyopelekea hata kupendwa na waalimu. Alikuwa Mr.Mwiba mwalimu mkuu msaisizi aliyewafundisha somo la hisabati. Alikuwa mkali kama mwiba. Mr. Mwiba alipambana na makundi ya wanafunzi walioiga tabia mbaya na kujitolea muda na wasaha wake wote kutokomeza makundi hayo ili kuikuza shule ile kitaaluma. Juhudi zake kuwasaidia wale wenye nia jna moyo wa kusoma hazikuhesabika. Kuna aliowafunza masomo ya ziada kwa kujitolea tu. Alisifika sana na kupendwa na wazazi na kujulukana kila pembe za mji wa Arusha. Wapo wazazi waliowaleta watoto wao waliosoma shule nyingine kuja kufundishwa na mwalimu huyu nyakati za likizo.
Mwaka 2000 mzee Majaaliwa alikuwa na hali ngumu kiafya. Japo alipata matibabu ya sukari kushuka. Alidhoofika kupita kiasi. Hakuweza tena kufuatilia maendeleo ya miradi na pia wanawe waliosoma. Alipopewa barua za kuitwa shuleni kwa akina Matochi aliwatuma kaka na dada zake wakubwa. Mwaka ukapita Matochi aliendelea na juhudi zake kama kawaida. Jioni alijiunga na wanafunzi wenzake kusoma kwa pamoja kwa njia ya mijadala. Mwishoni mwa wiki pia walikutana kujisomea na wenzake.
Haikuwa sababu ya Matochi kuendelea kufanya vema japo juhudi zilionekana. Waswahili husema gari bila dereva ni bure. Mwongozo wa waalimu bila msaada wa wazazi haukutosha ng’o!. Uchaguzi wa michepuo ulipofika hakuwahusisha wazazi kutokana na hali yam zee majaaliwa kuwa dhaifu. Alijichagulia mchepuo wa sanaa ambapo walisoma masomo ya biashara pia.
Matochi aliingia kidato cha tatu mwaka uliofuatia. Alibadilika mno kitabia. Hakuwa Yule Matochi wa zamanialiye pendwa na wengi. Alijiingiza katika makundi ya wanafunzi watukutu waliodiriki kuwatusi waalimu. Alijiona mpweke asiye na wazazi wala ndugu kwani maamuzi yalikuwa yake binafsi. Mama Lii hakuweza kuifuatilia vema elimu yake kwani hakuwahi kubahatika kuiona shule. Aliwahi kuhadithia wanawe juu ya tabia yake alipokuwa motto. Enzi za kale alipoamriwa kwenda shule alijificha vichakani na kurudi jioni nyumbani akijifanya ametoka shule. Japo alijua kusoma kwa utata na kuandika mwandiko duni. Ungeliufananisha na bata aliyechezacheza kandokando ya vidimbwi vya maji ya mvua. Alichoweza kusaidia ni kuhakiki ada imelipwa na Matochi kapata vitabu vya kuandika na sare za shule. Vingine havikumhusu.
Hali ya kutopata mwongozo na amasa za wazazi ilimfanya Matochi akate tama ya kusoma. Akawa hapendi shule kama awali. Alilimbikiza kazi za waalimu kwenye vitabu vyake. Hakupenda tena kuwa karibu na waalimu wake. Aliwaona waalimu kama chui. Alijijengea mazingira magumu ya kuwepo shuleni. Masikini moyo na jitihada vilimporomoka akawa mafano wa mwana mpotevu. Shuleni alihadhibiwa kwa kuchelewa na kufanya vibaya. Alikomaa utukutu na kiburi kwa kujibizana na waalimu. Ilikuwa kama mbwa nap aka. Hakuisha kupewa onyo kwa kusimamishwa masomo kwa muda.
Huo ulikuwa mwaka wa tatu. Angelikuwa mchezaji tungesema amenusurika kupewa kadi nyekundu na mwamuzi. Mitaani alijulikana kwa tabia mabaya za ulevi na uzinzi. Alijiingiza kimapenzi na kila msichana aliyemwona anamfaa. Wa kwanza alikuwa fatuma mwislam aliyekuwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba ya jirani na yao. Upole na umbile la mvuto vilimchanganya sana Matochi. Fatuma alipotembea aliyatingisha kwa madaha mithili ya bata aliyejishindia uwanja wenye maji taka. Alikuwa na umri usiozidi miaka 17 lakini tayari alishayajua mapenzi. Alikuja mjini kufanya kazi za ndani kwa kuwa hakuweza kuhitimu elimu ya msingi. Alisimamishwa masomo katika shule ya msingi ya Babati baada ya kupata ujauzito akiwa darasa la tano. Bahati aliyokuwa nayo ni uwezo wa kusoma maandishi ya Kiswahili chepesi na kuandika kwa taabu.
Matochi alipotoka shuleni alimsubiri Fatuma karibu na duka lililokuwa jirani na nyumba yao. Wakati mwingine alimuandikia barua na kuiacha pale dukani baada ya kuacha maagizo kwa kijana muuzaji aliyeitwa Mrombo. Mahusiano haya yaliota mizizi na kushamiri sana. Watu wote wa mtaa ule walijua kuhusu kilichoendelea baina ya wawili hawa. Matochi alikuwa na kikundi cha kujadili masomo ambacho walikutana na Elinami. Elinami alikuwa msichana aliyesoma shule ya upili ya Kimandolu. Alikuwa kidato kimoja na matochi japo shule tofauti. Walisoma na kuyajadili masomo pamoja kila siku nyakati za jioni. Matochi alipendwa sana na familia ya akina Elinami. Mama yake Elinami aliwahi kumfundisha Matochi wakati akiwa katika shule ya msingi. Matochi aliamua kuichukua fursa aliyoipata kama bahati. Aliita bahati kwani aliamini bahati haiji mara mbili. Wakiwa katika majadiliano na Elinami alimgusia masuala ya mapenzi. Elinami alipokataa aliacha kwenda kwenye majadiliano kwa kuwa alikuwa kichwa kilichotawala majadiliano yao. Alijaribu kumwandikia Elinami barua nyingi sana lakini hakupata majibu mazuri. Barua ya mwisho ilikuwa hivi;
Mpendwa Matochi,
Natumaini hujambo kwakuwa nami ni mzima wa afya.Dhumuni la waraka huu ni kutaka kukujulisha kwamba siwezi kuwa mpenzi wako kwani tayari nina rafiki ‘boyfriend’ tena hayuko mbali,nadhani unamjua. Unanishangaza sana kwani wewe pia unayo mpenzi ambaye ni Fatuma. Yaani kweli umekosa ‘demu!’ mtu mwenyewe anajichubua. Kwa taarifa yako Fatuma ni mke wa mtu. Ameletwa na mwajiri wake toka kijijini ili achukue nafasi ya mkewe aliyemfukuza. Kama uamini chunguza kwanini amemwamishia mjini alikofungua biashara ya hoteli. Tafuta demu mwingine Yule hakufai. Tena mtaa mzima mpaka watoto wanashangaa wewe una tembea na mke wa mtu.
Ni wako rafiki,
Elinami.
Baada ya kumaliza kuisoma roho ilimpasuka ghafla akabaki kapigwa bumbuwazi. Alihisi amegusa kinyesi cha binadamu. Alihofu habari zile zingeweza mfikia baba yake mzee Majaaliwa. Alipanga kuachana na Yule Fatuma. ‘mke wa mtu’ alikumbuka mstari katika barua ile aliyoandikiwa na Elinami.
Matochi alimwendea Mrombo na kumjulisha yale aliyoyasoma na kumwonya kutopokea tena barua toka kwa Fatuma. Huu ukawa mwanzo na mwisho wa Matochi kuwa na Fatuma. Alihisi haibu sana hakutaka tena kujihusisha kimapenzi na wasichana wa mtaani pale. Aliwaza sana na kujiona asiye na bahati ya penzi maishani mwake.
Aliupoteza muda wake mwingi kwa kutojisomea aliyofunzwa shuleni. Mtihani wa mwishoni mwa muhula alipata alama dhaifu sana. Aliwekwa miongoni mwa majina ya wanafunzi watukutu walioshindikana, tena waliotazamiwa kupata alama dhaifu kwenye mitihani ya mwisho
Akiwa kidato cha nne Matochi aliingia vijiweni kwenye madawa ya kulevya. Aliadhirika uraibu wa vileo vyote. Alikuwa mtoro wa vipindi aliyezoeleka na wanafunzi wenzake na pia waalimu. Muda wa kusoma aliutumia kufanya ulevi na kurandaranda mitaani. Walipofanya mitihani ya kujipima kidato cha nne alipata daraja la tatu. Alijipa moyo na kujisifu kwamba aliweza kuwashinda waliojiita wasongo wenye kuudhuria shule kila siku. Aliamua kuyachimbia madaftari na vitabu akisubiri mitihani ya mwisho ifike. Siku ya siku ikafika yeye na wenzake wakakaa kwenye mitihani ya kuitimu elimu ya sekondari. Alijitutumua kuwa mitihani ilikuwa kawaida na desturi yake ni kufanya vema kama alivyofanya katika mitihani ya kujipima Mock. Waliokuwa wasikivu wapole wanyenyekevu na wavumilivu walingoja mbivu. Waliopanda mbegu bora walitaraji mavuno mema. Wliokuwa watukutu wasiosoma wasumbufu nao walingoja hukumu. Mbaya zaidi hukumu ingeliwakuta wakiwa mitaani kunako washinda wengi wanaodiriki kupaita tambara bovu.
Matochi alipata fursa ya kufanya kila ovu alilojisikia kulifanya akiwa mitaani. Alilewa chakari akabebwa kwa machela akiwa taabani. Kazi nzuri kwake ilikuwa kuyasimamia matrekta yam zee Majaaliwa kwa kuhakikisha madereva wanafanya vile ipasavyo. Aliondoka asubuhi na kurudi jioni giza lilipoingia. Alijiita mzalishaji mali aliyehitaji pumziko na kujiliwaza kwa kupata moto au baridi. Saiku zilipita miezi ya hukumu ikafika. Wenye shinikizo la damu walianzwa. Wasiopenda redio wala jmagazeti walilazimika kujifanya wapenzi wa vyombo hivyo. Kumbukumbu za wosia aliopewa na mzee majaaliwa vilimwingia kichwani. “Mwanangu soma mimi sina uwezo wa kukusomesha shule binafsi tena”. Ilikuwa sauti yam zee majaaliwa enzi zake akiwa na afya njema iliyopenya katika akili na masikio ya Matochi kama ilivyokuwa hai.
Ilikuwa siku ya jumatatu usiku wa saa mbili. Matochi alikuwa katoka kutazama mechi kali ya miamba maasimu kati ya wanakijiji chao na kijiji jirani. Haikuwa kawaida yake kuwahi nyumbani mapema. Chakula cha jioni kililika bila yeye kuwepo nyumbani. Kama ilivyo desturi ya wengi wenye luninga kukaa ukumbini nyakati za jioni kutazama taarifa ya habari. “Matochi…matochi….matochi?” ilikuwa sauti ya kaka yake mkubwa kwa mama Lii aliyemwita kushuhudia matokeo yakisomwa na msemaji wa baraza la mitihani kwa vyombo vya habari. Daudi aliwaendea kama mkuki chumbani kwao kuwashtua juu ya matokeo kutangazwa. Matochi hakuwa mlevi siku hiyo ila alijiamini kupita kiasi. Alijua lazima angepita kama sio kwa daraja la kwanza basi la tatu.
Siku iliyofuata matochi alidamka asubuhi mapema kama kawaida huku akiwa na shauku ya kujua matokeo yake. Alitaka kwenda mjini lakini hakuwa hata na nauli wala hakujua yalikowekwa. SaaSaba na nusu mchana alipata lifti ya gari la jirani nakufika ofini ya afisa elimu mkoa wa Arusha kuyatazama matokeo. Kwa kawaida baada ya matokeo kutangazwa na baraza lenye makao yake Dar esa salaam hugharimu muda wa siku mbili au tatu kufika mikoani. Hivyo hakuyaona kwani hayakuwa tayari. Alirudi nyumbanii kwa miguu akiwa amekata tama kwa uchovu na njaa aliyokuwa nayo.
Alhamisi jioni, alikuwa Benguo aliyeleta kipande cha gazeti chenye majina ya matokeo ya watahiniwa wa mwaka 2002. Jina la Juhudi Majaaliwa lilikuwa katika kundi la wanafunzi waliopata daraja la nne. Moyo ulimpasuka ghafla kwa hofu kuu. Alishinda akiwaza nini cha kufanya kwa wakati uliofuatia. Ilikuwa mwisho wa safari ngumu ya usiku na mchana. Hakuna aliyeshughulika naye tena ukiachilia mbali mzee Majaaliwa aliyezoea kumtuma dawa zake za kujidunga kuongeza sukari mwilini za insulin.Alijifariji kwa kunywa pombe nyingi sana namadawa ya kulevya akijifanya kusahau machungu ya hukumu iliyosomwa.haikupita saa wala siku bila ya kupata aidha pombe au madawa yakulevya. Alidhoofika na kukonda kwa kutokula vizuri akawakama njiti. Aliwaza na kuwazuapasipo jibu alikumbuka idadi ya marafiki ilivyomfariji akiwa shule. Kwa wakati huo hakuna aliyemjali tena wote waliofaulu walijiunga na elimu ya juu katika shule walizopangiwa.kufuatia mienendo yake miovu idadi ya maadui ilikuwa kubwa zaidi ya marafiki. Sera ya kufanya lolote kupata chochote iliibuka mawazoni mwake. Aliamini pesa ndio msingi wa maisha hivyo aliisaka shilingi kwa udi na uvumba kila kukicha. Kwa kipindi kifupi baada ya zile kazi ngumu sura ilikunjamana na kumfanya aonekane kama mzee hali alikuwa na miaka 19 tu.Kwa kipindi chote cha mwaka 2003 alishindakuzunguka na magari ya mzee Majaaliwa akiwa kama utingo.
ITAENDELEA…..
Na Reginald Anderson
Ba Languages.

No comments:

Post a Comment