Thursday, September 27, 2012

MADHARA YA MICHORO MWILINI



Pichani ni bishost mrembo mwenye uraibu wa michoro ya tattoo akionyesha swag

By Reginald Anderson Mtui


Ebu fikiria kwa makini, ni sawa kwa mtu kuwa na shati moja maisha yake yote? Mmh utakuwa sahihi kabisa endapo jibu lako litakuwa si sawa kimtazamo wa wengi. Naam! hivyo ndivyo namna  michoro mwilini "tattoo" ilivyo, unachorwa mwili kwa wino usioweza kufutika kirahisi hivyo  alama/mchoro hubaki mwilini mwako daima. Kwa lugha ya kigeni michoro hii hujulikana kama “tattoo” kwani hutokana na neno la “kitahiti” litamkwalo “tatu” kwa maana ya  alama ya kudumu inayobuniwa na kuchorwa kwenye  ngozi kwa kutumia rangi za aina mbalimbali. Siku hizi michoro hii huchorwa kwa kutumia sindano na kifaa cha kisasa cha umeme chenye sindano kinachotoboa tabaka la juu la ngozi (dermal layer) kirahisi na kufanya mchoro au alama za aina Fulani. Vifaa hivi kitaalamu tunaviita "rapid-injection-electronical device". Katika insha hii nitabainisha kwa kina madhara yaletwayo na michoro hii ambayo imepewa kipaumbele na jamii ya sasa hosusani vijana.  Ndiyo waweza kupata madhara  kiafya, kimtazamo wa jamii inayokuzunguka, na hasara zisizo za lazima kiuchumi.

Athari Kiafya
Afya bora ni muhimu sana. Ndiyo maana unashauriwa kuwa makini kabla ya kuchukua uamuzi wa kujichora. Ni vema kutembelea vituo vya kujichora "studio" nyingi na kuhakikisha unachagua zile zinazotoa huduma bora zinazofuata taratibu za afya. Ni lazima studio iwe na vifaa vya kusafisha nyenzo za kazi kitaalamu tunaziita “outoclave” au “medical sterilization machines” ambavyo hutumia joto kali kuvipasha vitendea kazi yaani mashine inayotoboa ngozi na kadhalika. Pia hakikisha sindano zote zinazotumika kwa kazi hii ni mpya kwa kufungua paketi zenye nembo na tarehe. Hivi sasa kuna wataalamu bandia wanaofanya kazi hizi za uchoraji pasipo vibali wala vifaa muhimu vya kufanyia kazi hizo. Hivyo kuwa makini sana na watu wa aina hii. wino unaotumika kuchorea michoro hii huwekwa ming’aro ya chuma "dyes" ambayo huweza kuwa na  sumu hatari kwenye ngozi ya binadamu. Wino mweusi waweza kusababisha saratani ya ngozi "skin cancer". Madhara mengine ya michoro hii ni uvimbe kwenye ini "Hepatitis". Pia kuna uwezekano wa kupata Ugonjwa wa Ukimwi "HIV-Aids" ikiwa vifaa vitumiwavyo kuchorea havisafishwi vizuri kwa mashine.

Mtazamo hasi katika jamii
Tatizo lingine la michoro hii ni mtazamo hasi kutoka kwa jamii inayopinga michoro na nembo za aina hii. Kumekuwepo na uvumi kutoka kwa jamii kuhusu makundi ya watu wanaochora michoro hii kuwa ni wale wanaojihusisha na vitendo viovu vya kinyama, kihuni au kikatili. Katika ofisi mbalimbali za kazi waajiri hukataa kutoa ajira kwa watu wenye michoro na nembo hizo. Kumekuwepo na visa vya wazazi kuwakataa watoto wao kwa kuwa wamejichora michoro hiyo. zipo baadhi ya sehemu za kujipatia huduma ambazo haziruhusu wateja wake kuingia huku wakeka wazi michoro hiyo; mfano katika mikahawa ya vyakula na hoteli mbalmbali duniani.

Athari za Kiuchumi
Kwakweli michoro hii ikifuata taratibu za kiafya zinazo kubalika mchorwaji hulazimika kutoa fedha nyingi kuliko maelezo. Studio nyingi zimeonyesha takwimu za gharama ya kuchora michoro hiyo kwa saa moja ni zaidi ya $100 (Dola mia moja) hivyo ukihitaji tatoo kwa masaa manne au zaidi ni fedha nyingi mno. Zipo gharama zinazolipwa ikiwa mchoro umemsababishia mhusika maambukizi. Hizi ni gharama za kununua madawa ya kutibu ngozi (vidonda).



Pichani ni muathiriwa wa michoro ya tattoo


Na mwisho, nawashauri(wasomaji wangu) kuchukua taadhari kabla ya kufanya uamuzi wa kujichora. Kujua pa kuchorea na umuhimu wa kuchora michoro hiyo. Ili tuishi vema ni lazima tuwe na mahusiano mazuri na jamii zetu. Tunaposababisha tofauti na familia zetu ni tatizo kubwa sana kwani tutafanya maisha yetu kuwa ya wasiwasi yasiyo na furaha wala amani daima.